HADITHI ZA SHIGONGO



The Last Breath - 1
Mwaa!” Loveness alimbusu Johnson kwenye paji la uso, kisha akageukia upande wa pili na kumbusu shavuni mtoto wao Melania, binti yao mwenye umri wa miaka mitatu!
Moyoni mwake alisikia uchungu mno, hakuna kitu alichokichukia kama kuagana na watu aliowapenda. Kwa hakika mume wake Johnson na binti yake Melania, ndiyo walikuwa watu pekee aliowapenda kuliko wengine wote chini ya jua la Mungu.
Kwa nguvu zake zote alijitahidi kuyazuia machozi yasimlengelenge lakini haikuwezekana, taratibu yakazipenya kope na kuanza kushuka kuelekea mashavuni, Johnson akachukua kitambaa mfukoni kwake na kuanza kumfuta huku akimtuliza asiendelee kulia mbele ya mtoto.

“Mpenzi si utakuja nyumbani kwenye Sikukuu ya Krismasi?”
“Ndiyo.”
“Kuanzia sasa mpaka Krismasi bado siku ngapi?”
“Kama mwezi mmoja hivi.”
“Sasa kwa nini unalia?”
“Sijielewi, moyoni mwangu nahisi kama nawaona kwa mara ya mwisho!” Loveness aliongea na kuzidi kububujikwa na machozi.
“Mama acha kulia!” Melania alimwambia mama yake na kumfanya ajisikie vibaya.
Katika maisha yake yote tangu azaliwe, Loveness alishasindikiza watu wengi sana stendi za basi, viwanja vya ndege, bandarini waliokuwa wakiondoka na kumwacha, ni kweli aliumia na kusikitika na ndiyo maana alizichukia sana sehemu hizo, lakini siku hiyo aliumia zaidi kuliko siku nyingine zilizotangulia, kuna sauti ilimwambia kutoka ndani kabisa kwamba asingewaona tena lakini alibishana nayo.
“Kwa kweli ungekuwa uwezo wangu, ningewazuia msisafiri!”
“Kwa nini?”
“Najisikia vibaya mno Johnson, nahisi kuna tatizo litatokea!”
“Hapana,  hizo ni hisia tu mpenzi! Acha nimrudishe Melania Dar es Salaam, Jumatatu anatakiwa darasani, si unajua likizo yenyewe ilikuwa ni ya wiki moja tu, tumekuona mpenzi, utatukuta Dar es Salaam utakapokuja na safari hii ninataka nikufanyie ‘sapraizi’ ambayo hutaisahau maishani mwako!”
“Sapraizi gani?”
“Wewe utaona ukija, siwezi kukuambia sasa hivi!” Johnson aliongea, ingawa moyoni mwake alielewa alitaka kumnunulia mke wake gari mpya aina ya Range Rover Evoque.
Zamu yao ya kuingia uwanjani ikafika,  hawakuwa na namna tena ya kuendelea kubaki nje, muda wa kuiacha Kinshansa ulikuwa umefika na pia kumwacha Loveness peke yake akiendelea na kazi katika Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambalo ofisi zake zilikuwepo katika jiji hilo,  alikofanya kazi kama Afisa Ustawi wa Jamii.
Loveness alimwangalia Johnson machoni, akahamishia tena kwa mtoto wake, akakosa nguvu za kuwaangalia, akainamisha uso wake chini, machozi yakadondoka sakafuni! Alichokifanya Johnson ni kujiondoa kwenye foleni, asingeweza kuondoka na kumwacha katika hali hiyo, akamkumbatia kwa mkono wake wa kuume kisha kumtaka afumbe macho yake ili wamwombe Mungu pamoja.
“…Mungu mwema, ubaki na mke wangu mpaka tutakapokutana naye tena, unajua ni kiasi gani nampenda na ningetaka kubaki hapa Kinshasa pamoja naye, lakini haiwezekani sababu ya majukumu yaliyoko nyumbani, hivyo basi namwacha mikononi mwako, nasi tubariki katika safari yetu mpaka tufike Dar es Salaam…” Johnson alimaliza sala yake na kumpiga busu Loveness usoni kwake.
Kilichofuata baada ya hapo ni kuingia uwanjani ambako walikaguliwa mizigo yao pamoja na wao wenyewe, kabla hawajaingia ndani kabisa Johnson akiwa amembeba Melania, aliangalia nje na kumwona Loveness amesimama palepale walipomwacha, mwanamke mmoja akionekana kumbembeleza aache kulia.
“Mama bye!” Melania aliongea kwa sauti ya juu mpaka watu wengine wakageuka.
“I love you Melania!”
“I love you to mom!”
“Take care of yourself and listen to teacher Joyce in the class, okay?” (Ujichunge na msikilize mwalimu Joyce darasani, sawa?)
“Yes mom, I will.” (Ndiyo mama, nitafanya hivyo!)
“Bye baby!” (Kwaheri mpenzi!)
“Bye husband!” (Kwaheri mume wangu!)
Johnson na mtoto wake wakazama ndani ya uwanja ambako walikuta pilikapilika za watu wakikimbia huku na kule kujaribu kuwahi ndege zao, moyoni mwake Johnson alisumbuliwa sana na alichokionyesha mke wake uwanjani, yeye mwenyewe akaanza kuingiwa na aina fulani ya hofu lakini akamwamini Mungu na kutembea moja kwa moja hadi chumba cha kusubiria ambako walikuta tayari abiria wa ndege yao wamekwishaanza kupanda.
Loveness hakuondoka uwanja wa ndege, alichokifanya ni kusogea nyuma kidogo kuliacha jengo la uwanja katika sehemu ambayo angeweza kuziona vizuri ndege zilizoruka. Dakika ishirini na tano baadaye aliiona ndege ndogo ya Shirika la Ndege la Kongo, yenye uwezo wa kubeba abiria hamsini ikiruka, hiyo ndiyo Johnson na Melania walipanda, akanyanyua mikono yake juu na kumwomba Mungu aepushe kile ambacho moyo wake ulikuwa  ukikihisia.

***
Ndege ilishaacha sehemu ya mawingu, Johnson na mwanaye Melania walikuwa wameketi vizuri kwenye viti, mkononi Melania alikuwa akichezea michezo ya kompyuta kwenye IPad. Tayari walishatangaziwa kwamba ishara za  mikanda zilishaondolewa, hivyo  waketi vizuri kwenye viti vyao na kufurahia safari.
Walikuwa wakipita kwenye futi ishirini na tano elfu juu ya usawa wa bahari, hali ya hewa ilikuwa safi kabisa, ndege imetulia kama vile walikuwa sebuleni nyumbani kwao. Wahudumu wa ndege waliwafikia na kuwauliza kile walichohitaji kutumia, Johnson akaagiza chai na kwa ajili ya mtoto wake akaagiza juisi ya sharubati pamoja na pakiti ya korosho.
Juisi zilipowekwa tu juu ya meza, ghafla mlipuko mkubwa sana ukatokea na harufu ya kama kitu kilikuwa kinaungua ikasikika! Abiria wote ndani ya ndege wakapatwa na mshtuko na kelele zikaanza kusikika, ingawa wafanyakazi ndani ya ndege hiyo walijitahidi kama hapakuwa na kitu kilichotokea kwa kuweka tabasamu usoni, abiria walishagundua kwamba tatizo kubwa lilikuwa limetokea.
Troli lililobeba chakula na vinywaji likaanza kusukumwa kuondolewa katikati mpaka sehemu yake, wahudumu wakaketi kwenye viti na kufunga mikanda, abiria wote wakatakiwa kufanya hivyo. Sekunde chache baadaye sauti ya rubani ikasikika akiwaeleza kwamba injini moja ya ndege yao ilikuwa imelipuka na kusimama kufanya kazi, hivyo walikuwa wanatumia injini moja tu, akawatuliza kwa kuwaambia wasiwe na wasiwasi kwani kwa injini moja wangeweza kufika angalau Bujumbura ambako wangetua kwa dharura.
Watu wakatulia kidogo baada ya kuelezwa maneno hayo, haikuwa hivyo kwa Melania ambaye alikuwa akilia kwa nguvu huku akitaja jina la mama yake. Kazi ya Johnson ikawa ni kumtuliza na kumwambia kila kitu kingekuwa sawa, ingawa kichwani mwake akielewa kabisa walikuwa katika hatari na kwamba kumbe Loveness alikuwa ameona kitu kilichokuwa kinakwenda kutokea.
Hali ilikuwa mbaya, ndege sasa ilikuwa ikienda kwa mwendo wa taratibu kuliko mwanzo huku harufu ya kitu kilichokuwa kinaungua ikisikika na moshi ukiingia ndani ya ndege kiasi cha watu kuanza kukohoa. Melania alikohoa sana pengine kuliko watu wengine, Johnson akachanganyikiwa kabisa.
Vifaa vya kupumulia vikashuka kutoka eneo la juu la kuhifadhia mizigo, Johnson akachukua kimoja na kumvisha mtoto wake kisha yeye mwenyewe kuvaa cha kwake, vikasaidia kidogo katika upumuaji. Ghafla ndege ikaanza kuyumba kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Dakika kama kumi hivi baadaye mlipuko mwingine wa pili ulisikika tena, moshi ukazidi ndani na ndege badala ya kwenda mbele ikaanza kushuka kwenda chini! Sauti iliyosikika kupitia kwenye kipaza sauti ilikuwa ni ya rubani akiwatangazia abiria kwamba injini zote za ndege zilikuwa zimelipuka na sasa ndege yao ilikuwa ikienda chini kwa kasi ambako ingejipiga chini.
“Kila mmoja wetu anaweza kusali kwa dini yake, pengine Mungu anaweza kutunusuru!” ilikuwa ni sauti ya rubani.
Hapo ndipo Johnson akaelewa kwamba kweli walikuwa wanakufa, akamsogeza mtoto wake karibu na kuanza kulia huku akimwomba Mungu atende muujiza wowote ambao angeweza, taswira ya Loveness akilia uwanja wa ndege iliendelea kumwijia, akajuta ni kwa nini hakumsikiliza.
“Dad are we going to die!”(Baba, tunakufa?)
“No! We can’t die, just pray!”(Hapana, hatuwezi kufa, sali tu!) Johnson alimwambia Melania ingawa alikuwa na uhakika kabisa kilichosemwa na mtoto wake kilikuwa kweli.
Ndege ilikuwa ikishuka kwa kasi mno kiasi cha kuhisi utumbo ulitaka kupitia mdomoni, Melania alikuwa akilia kwa nguvu na kuita jina la mama yake.
***
Nisingependa kumaliza hadithi hii ya leo bila kukumbusha jambo muhimu la kutoa maisha yako kwa Mungu. Maisha tuliyonayo hapa duniani ni mafupi sana, yanapita kama maua yachanuavyo na kunyauka. Wengi unaowafahamu wamekufa lakini wewe unapumua, ni vyema basi kufikiria maisha baada ya kifo.
Kila siku jiulize: “Hivi nikifa leo nitakwenda jehanam au peponi?” Kila mmoja wetu analo jibu lake, bila shaka sote tungependa kwenda peponi. Kama hivyo ndivyo, basi tiketi ya kwenda huko ni matendo mema na kujiepusha na uovu.
Tukumbuke mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele.

Je, nini kitaendelea katika hadithi hii ya kusikitisha? Watakufa?.

7 comments: