BURUDANI

KANUMBA DAY: HISTORIA KUANDIKWA J’TATU

TUKIO kubwa na la kihistoria linatarajiwa kuandikwa Jumatatu ijayo katika maadhimisho ya Siku ya Kanumba katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagala-Zakhem jijini Dar.

Marehemu Steven Kanumba enzi za uhai wake.
Historia hiyo itaandikwa na mastaa wa Bongo Movies, Bongo Fleva, Taarab na Dansi huku mgeni rasmi Meya wa Ilala, Jerry Slaa akishuhudia na yeye kuwa sehemu ya historia hiyo inayofanyika kila mwaka.
Frederick Mwakalebela ambaye ni mmoja wa waratibu wa maadhimisho hayo, amesema siku hiyo itakuwa ya kukumbukwa kwani mbali na matukio ya kumkumbuka marehemu na mchango wake katika tasnia ya filamu, burudani itakuwepo.
Amesema Mzee Yusuf na bendi nzima ya Jahazi wataporomosha nyimbo zao zote kali, Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’, Chegge, Snura, Juma Nature kwa nyakati tofauti watalishambulia jukwaa kushusha burudani ambayo haijawahi kutokea.
“Itakuwa ni huyu anapanda huyu anashuka jukwaani, hakuna muda wa kupumzika, niwasihi wapenzi wa filamu na burudani kwa jumla, wafike kwa wingi ili tuweze kuifanikisha Kanumba Day 2014 kwa heshima kubwa,” alisema Mwakalebela.
Usiku huo unatarajiwa kupambwa na idadi kubwa ya mastaa, kutakuwepo na zulia jekundu ambapo mashabiki wataweza kupiga picha na mastaa mbalimbali, kuzungumza nao na mwisho wa siku burudani zote hizo zitakamilika kwa kiingilio cha Sh. 10000 tu!
Utakosaje?!

No comments:

Post a Comment