Friday 4 April 2014

GOLDEN TEARS(MACHOZI YA DHAHABU)

MWANDISHI mmoja maarufu wa habari za michezo na burudani nchini Tanzania, aitwaye Saleh Ally akiuelezea uzuri wa msichana huyo aliposhiriki shindano la urembo la nchi hiyo akiwa na umri wa miaka kumi na sita mwaka 2006, ingawa maneno ya kalamu yake sijui kama yalitosha kuuelezea uzuri wa msichana huyo aliwahi kuandika:
…ni mrefu mithili ya twiga, ana shingo ndefu kama ya mbuni, kiuno chembamba mithili ya nyigu, vilima viwili chini ya kiuno chake upande wa nyuma sawasawa na vilele vya mlima, sehemu ya kushoto na kulia chini ya kiuno alikuwa na vivimbe vikubwa viitwavyo hips vilivyomfanya awe kama punda aliyebebeshwa mzigo kila upande. Hakuwa na tumbo kabisa, sawasawa na runinga mpya ya Samsung iitwayo ‘Flat Screen’, kifuani kwake kwa mbele alikuwa na vilima vingine viwili vyenye ukubwa wa tikitimaji la kati ambavyo ingawa alikuwa mwembamba alihitaji sidiria kubwa. Rangi yake ya ngozi ilikuwa maji ya kunde, midomo yake minene ya duara, pua yake ndefu ingawa butu kidogo kwa mbele, macho makubwa kama ya mtu aliyetaka kusinzia, mashavuni alikuwa na kishimo kimoja kila upande ambavyo alipocheka viliongezeka kina, hivyo vinaitwa dimpoz. Pamoja na kuwa mwembamba, kwa chini alikuwa na mguu mzito, ambao wengi waliuita mguu wa Kirinyota mgenzi au Primus, bia maarufu nchini Rwanda. Hata kama maelezo ya mwandishi huyu hayakutosha kubeba ujumbe wote juu ya uzuri wa msichana huyo, maneno yanayotosha kumwelezea ni kwamba alikuwa ni msichana mrembo mno na kivutio kwa kila mtu aliyemwangalia, si wanawake wala wanaume. Kama kuna binadamu yeyote aliyetaka kuthibitisha uwezo wa Mungu wa kuumba viumbe vizuri, alichotakiwa kufanya ni kukutana na msichana huyu ambaye watu wengi walipenda kumwita Bongo Cinderella, ingawa jina lake halisi lilikuwa ni Goodness Masanja. Hakuna kizuri ambacho hakina mtu wa kuzichukua sifa, wengi walisema uzuri wa Goodness ulikuwa ni zawadi kutoka kwa mama yake mzazi ambaye hakika pamoja na umri wake mkubwa alikuwa mrembo kupindukia, umbile lake pia liliwafanya hata vijana wa umri mdogo kabisa waseme: “Yule mama akinikubali, mimi sijali umri wake, namuoa,” wakiwa wamepuuza kabisa ukweli kwamba mama Goodness, alikuwa mke wa mtu tena kigogo serikalini. Pamoja na uzuri wote, Goodness alijawa na vipaji vingi sana na aliamini njia pekee ya kufanikiwa maishani, haikuwa kukaa darasani peke yake bali mtu angeweza kutumia kipaji chake na kufika juu ambako angekutana na wengine waliochagua kupitia njia ya elimu kufika hukohuko juu. Kwa sababu hiyo hakuendelea sana na masomo hadi chuo kikuu, alichofanya ni kuufuata moyo wake kwa kushiriki shindano la urembo la Tanzania na kufanikiwa kuwa Miss Tanzania na kwenda kushiriki mashindano ya urembo wa dunia yaliyofanyika Warsaw nchini Poland. Mwaka mmoja wa taji lake ulipomalizika, Goodness aliingia kwa miguu miwili katika uchezaji wa filamu, kazi ambayo ndani ya muda mfupi ilimfanya apande daraja na kuwashinda hata wasanii waliokuwepo kwa miaka mingi kabla yake akiwa mtoto, kufumba na kufumbua akawa anaingiza mamilioni ya fedha kupitia tasnia hiyo. Haikuwa fedha tu iliyoingia maishani mwake, bali pia umaarufu wake uliongezeka maradufu. Goodness akawa mtu wa kufuatwa na kamera za mapaparazi kila alikokwenda, hapakuwa na kitu alichokifanya ambacho hakikuonekana habari. Hata alipotema mate chini, alipigwa picha na siku iliyofuata sura yake ilikuwa kwenye ukurasa wa mbele wa Magazeti Pendwa nchini Tanzania yakinunuliwa kama njugu. Goodness akabadilika na kuwa bidhaa. Alionekana ni msichana mwenye furaha muda wote kwa sababu ya tabasamu alilokuwa nalo na sauti yake nyembamba aliyoitoa kila alipoongea, akibadilisha magari ya kifahari kila siku. Hakika aliogelea kwenye utajiri wa kutafuta mwenyewe akiwa na umri mdogo. Siku zote tangu akiwa mtoto, aliamini fedha ilikuwa ni chanzo cha furaha maishani, kwamba mtu mwenye fedha nyingi ana uwezo wa kununua chochote hivyo maisha yake siku zote yalijaa furaha, cha kushangaza akiwa na utajiri wote aliokuwa nao, bado ndani ya moyo wake, Goodness hakuwa na furaha, jambo ambalo watu wengi hawakulifahamu na hakutaka kulionesha wazi. Aliishi kwenye nyumba kubwa ya kifahari, peke yake pamoja na mbwa wake mdogo mweupe, Pogo, ambaye alimpenda kupindukia na ndiye alikuwa faraja ya moyo wake kila alipopatwa na huzuni au kuumizwa na mtu yeyote. Alimvisha nguo za thamani na kumpulizia manukato ya bei kubwa na ndiye aliyelala naye chumbani, kiasi cha baadhi ya watu kuhisi pengine alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi, sababu hawakujua nani hasa alikuwa mpenzi wake. Kwa Goodness, Pogo hakuwa mbwa kama watu wengi walivyomchukulia, alikuwa mtoto kama ambavyo akina mama wengi huwa na watoto wao! Alikwenda naye kila mahali ndani ya gari lake na aliposhuka alitembea akiwa ameshika mnyororo wake na wakati mwingine alimbeba kwenye mkoba, jambo lililofanya kila alikopita watu wasimamishe shughuli zao na kumwangalia. Alipenda watoto tangu utotoni mwake, zawadi ambazo alipenda wazazi wake wamletee zilikuwa ni midoli ya watoto ambao aliwabeba mgongoni kama ambavyo watu wengi hubeba watoto na kuwabembeleza mpaka alipoamini wamesinzia na kuwalaza, walipoamka aliwaogesha na kuwalisha. Kuna wakati suala la kufanya kazi za shule lilikuwa ni la kulazimishwa kwa sababu muda mwingi aliutumia kutunza midoli yake. Alipopata mafanikio makubwa kifedha maishani mwake akiwa na umri mdogo, kwa sababu alikuwa hajampata mwanaume wa kumpenda na kuzaa naye mtoto, Goodness aliamua kumchukua Pogo na kumfanya mwanaye, tangu siku hiyo maisha yake yalibadilika, akajisikia mama mwenye mtoto, alimdekeza Pogo kuliko kitu kingine chochote. “I don’t want to get married, but I need my own kid!”(Sitaki kuolewa lakini nataka kuwa na mtoto wangu!) aliwaza Goodness katikati ya usiku, baada ya kusoma habari mtandaoni mtu akiwa ametoa maoni yake na kusema eti alikuwa tasa, asingekuwa na mtoto kabisa maishani mwake ndiyo maana aliishi na mbwa kama mwanaye, kauli hiyo ilimuumiza sana na kumfanya alie mfululizo. “I am going to prove to the hatters that I am not barren!”(Nitawathibitishia wenye chuki zao kwamba mimi si tasa!) alijisemea moyoni mwake Goodness akiwa amepania kumtafuta mtoto kwa gharama yoyote. Kilichofuata baada ya hapo zilikuwa ni juhudi za kutafuta mtoto kwa gharama yoyote ile bila kujali dunia ingesema nini ili mradi yeye alitaka apate mtoto wake wa kike, uamuzi huu ndiyo ulimfanya Goodness apuuze dunia ingesema nini juu yake na kuanza kutoka na wanaume mbalimbali kimapenzi akitafuta furaha ya moyo wake; mtoto. Kwanza kabisa alianzisha uhusiano na msanii mmoja wa muziki wa kizazi kipya, aliyesifika kwa kuwa na tabia mbaya lakini Goodness hakujali, alichotaka yeye ni kupata mimba ili azae mtoto wake. Kijana huyu akiwa haamini kwamba hatimaye alikuwa amefanikiwa kumlaza kitandani na kufanya ngono na msichana mrembo kama Goodness, alimpiga picha za video na kuziweka mtandaoni ili dunia yote iamini kwamba yeye ni kidume. Picha hizo zilisambaa sana ndani ya muda mfupi na baadaye kuingia kwenye Magazeti Pendwa, kila Mtanzania akaziona na jina la Goodness likachafuka. Kila siku akawa anaandikwa juu ya picha hizo, jambo lililomuumiza sana na kumfanya ajifungie ndani ya nyumba yake akilia. Kitendo hicho kilisababisha familia yake yote ijumuike kumfariji ili asichukue uamuzi mbaya ya kukatisha uhai wake, jambo aliloongelea kulitenda. Kwa kijana aliyesambaza habari hizo, ilikuwa ni fahari kubwa bila kujali alimuumiza mwenzake kiasi gani, wiki chache baadaye, hali ilitulia kidogo, watu wakasahau kilichotokea na cha kushangaza zaidi upendo wa Watanzania kwa Goodness uliongezeka zaidi ya ilivyokuwa mwanzo, kila alikopita watu walimfurahia na kuomba kupiga naye picha, jambo ambalo halikutokea kabisa kwa wasanii wengine. Tukio hilo ndilo lilifikisha mwisho uhusiano kati ya Goodness na msanii huyo mpenda sifa, lakini kwa sababu alikuwa hajatimiza lengo lake la kupata ujauzito, aliamua kukubali uhusiano na mwanamuziki mwingine maarufu ambaye naye kama ilivyokuwa kwa yule wa mwanzo, alisambaza habari hizo kwenye magazeti ili kujipatia umaarufu na kupandisha jina lake maana ilionekana kama vile Goodness alikuwa na nyota ya kusaidia watu wengine kung’ara. Kitendo hicho kilimfanya aachane na huyo pia, hivyo ndivyo maisha yake yalivyoendelea akisaka mtoto lakini nyakati zote hakuanzisha uhusiano na wanaume kwa wakati mmoja, alipoachana na huyu ndiyo alianzisha uhusiano na mwingine lakini kwa sababu alikuwa maarufu na Magazeti Pendwa yaliandika sana habari zake kubadilisha wanaume, Goodness alitafsiriwa kama malaya. Jambo la muhimu alilolifanya ili kuepuka kuyaingiza maisha yake kwenye hatari ya kupata Ukimwi hata kama angempata mtoto, ni kuwashawishi wanaume wote aliokutana nao na kuanzisha uhusiano, kwenda kupima damu zao kabla hawajakutana kimwili, hii ilimpa nafasi kubwa sana ya kujiepusha na gonjwa hilo hatari. “Sitaacha mpaka nipate mtoto wangu mwenyewe!” alijisemea maneno hayo. Baada ya kutoka na vijana wengi wenye majina makubwa na wapenda sifa akitafuta mtoto, hatimaye Goodness alifikia uamuzi wa kuachana nao na kuanza kutoka na wanaume watu wazima, bila kujali walikuwa na ndoa zao au la! Alichokitaka yeye ni mwanaume wa kumpa mtoto, basi.

No comments:

Post a Comment