Sunday 13 October 2013

WAHAMIAJI HARAMU WAKAMATA MOROGORO

Wahamiaji haramu 16 wakamatwa Morogoro
JUMAPILI, OCTOBA 13, 2013 05:18 ROSE CHAPEWA NA MERINA ROBERT, MOROGORO
*Walikuwa ndani ya lori la chokaa
WATU 16 wanaodhaniwa kuwa ni wahamiaji haramu kutoka nchi mbili za Somalia na Ethiopia, wamekamatwa wakiwa wanasafirishwa kwenye lori lililosheheni mzigo wa chokaa, huku baadhi yao hali zao zikiwa mbaya kutokana na kukosa hewa.

Wahamiaji hao haramu walikamatwa jana katika barabara kuu ya Morogoro – Iringa, huku wakiwa wamefunikwa na turubai katikati ya mzigo wa chokaa inayotengenezwa na kampuni ya Hydrated lime ya jijini Tanga.
Inadaiwa kuwa chokaa hiyo ilikuwa ikisafirishwa kupelekwa katika nchi za Zambia na Afrika Kusini, ambapo ilikuwa ikisafirishwa na lori lenye namba za usajiri T 707 CGY, mali ya kampuni ya Silent Road Haulage Ltd ya jijini Dar es Salaam.
Aidha baadhi ya mashuhuda, akiwemo Godfrey Chambo na Ofisa Uhamiaji Wilfred Minja, walisema walibaini kuwepo kwa wahamiaji hao kwenye gari hilo, baada ya mmoja wao kuanguka kutoka kwenye gari hilo.
“Gari hili lilisimama kwenye kituo cha mafuta cha Oil Com kilichopo Nane Nane kwa ajili ya kulisafisha, baada ya dereva kumaliza kufanya usafi na kutaka kuondoka, ndipo mhamiaji mmoja alianguka kutoka kwenye gari hilo,” alisema Chambo.
Walisema kuwa baada ya kuanguka, dereva wa gari hilo alianza kumpiga mateke na kumtaka aingie kwenye gari na baadaye dereva huyo alimnyanyua na kumuingiza kwenye gari, kitendo ambacho kilishuhudiwa na watu mbalimbali, wakiwemo madereva wa pikipiki, maarufu kama boda boda.
Katika kuonesha ushirikiano, madereva wa pikipiki walilikimbiza gari hilo na kufanikiwa kulisimamisha, huku dereva wa lori lililobeba wahamiaji hao akikataa kusimama hata aliposimamishwa na askari wa usalama barabarani.
Maelfu ya mashuhuda waliojitokeza kituo kikuu cha polisi na waendesha pikipiki waliolisindikiza lori hilo hadi kituo kikuu cha polisi, walilaani kitendo hicho kinachofanywa na madereva wa malori kubeba wahamiaji haramu kuwa si cha kiungwana.
Hata hivyo wananchi waliojitokeza na kusaidia kuwakamata watuhumiwa hao na kuwashusha katika Kituo Kikuu cha Polisi, walilalamikia kutelekezwa na Jeshi la Polisi pamoja na watu wa Uhamiaji kwa kutowapa chochote, pamoja na kwamba walijitolea na kuumizwa na chokaa iliyosheheni katika lori hilo. Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile kwa ajili ya kuthibitisha tukio hilo, hakupokea simu yake kiganjani.

No comments:

Post a Comment