Sunday 13 October 2013

VIJANA TUAMKE ILI TUKOMBOE TAIFA LETU

Dk. Bilal: Taifa linakabiliwa na uhaba wa wakunga


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal, amewaomba wadau wa maendeleo nchini kuunga mkono jitihada za serikali za kuokoa uhai wa mama na mtoto. Wito huo aliutoa jijini Dar es Salaam juzi usiku, katika hafla ya chakula cha hisani kilichoandaliwa na Shirika la AMREF Tanzania, kwa lengo la kuchangisha fedha za kusomesha wakunga 3,800.

Dk Bilal alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye uhitaji mkubwa wa wakunga, hasa katika maeneo ya vijijini, ambako kumekuwa na ripoti nyingi za vifo vinavyotokea wakati mama anapojifungua.


“Naunga mkono kampeni hii ya Simama Mama wa Kitanzania, naamini itakuwa chachu kwa wadau wote wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizi za kuokoa uhai wa maisha ya mama na motto, kwa sababu kuna vifo vingine vinaweza kuzuilika kama kutakuwa na wakunga wa kutosha,” alisema Dk. Bilal.

Naye Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete, alisema jukumu la kuokoa maisha ya mwanamke wakati wa kujifungua ni la Watanzania wote, hivyo aliitaka jamii kuipa umuhimu kampeni hiyo ya Simama Mama wa Kitanzania, yenye lengo la kutoa elimu ya ukunga kwa vijana 3,800, ifikapo mwaka 2015.

“Watanzania tupo milioni 44, kama nusu ya watu wote wakichangia angalau Sh. 100, kampeni hii itakuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, japokuwa kuna uhitaji mkubwa wa wakunga nchini, kampeni hii itakuwa imeonesha nia ya kulimaliza tatizo hilo,” alisema Mama Salma Kikwete.

Kwa upande wake, mwakilishi wa AMREF nchini, Dk Ritta Ameron, alisema mpango huo wa kusomesha wakunga 3,800 utagharimu dola 3,000 kwa kila mwanafunzi.

Alisema, tayari wanafunzi 10 kutoka Wilaya ya Kilindi wameshaanza kupata mafunzo hayo katika Chuo cha Uuguzi cha Muheza, chini ya ufadhili wa Benki ya Barclays Tanzania.

Katika hafla hiyo, wadau mbalimbali wa maendeleo walifanikiwa kuchanga Sh milioni 719, lengo likiwa ni kutunisha mfuko wa kampeni hiyo.

No comments:

Post a Comment