Sunday 13 October 2013

MAGUFULI: HATA KAMA SIRIDHISWI NATII MAELEKEZO YA PINDA


Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
HATUA ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kubatilisha uamuzi wa Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, uliosababisha mgomo wa malori na mabasi nchini, imeanza kuchukua mwelekeo mpya, baada ya Waziri huyo kusema anatii kile alichokieleza kiongozi wake huyo, hata kama hakuridhishwa nacho.

Agizo la Pinda lilikuja baada ya Magufuli, kutangaza kuanza kutumika kwa kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 2001, inayotaka malori yote yanayozidisha uzito uliopo ndani ya asilimia tano kupunguza mzigo, kupanga mzigo upya au kulipia uzito uliozidi mara nne ya tozo ya kawaida.

Akizungumza na RAI Jumapili kupitia kwa Katibu wake, Martyin Ntemo, Waziri Magufuli alisema licha ya agizo hilo la Waziri Mkuu, msimamo wake ni kufanya kazi na kampuni zinazoheshimu sheria na si vinginevyo.



“Maamuzi ya Waziri Mkuu hayawezi kupingwa au kuhojiwa, natii kile kilichoelekezwa, hata kama sijaridhishwa moyoni mwangu…ila msimamo wa Wizara yangu ni kufanya kazi na kampuni zinazoheshimu sheria na si vinginevyo,” alikaririwa Magufuli.Kauli hiyo ya Magufuli inadhihirisha wazi kwamba hajaridhishwa na agizo la Waziri Mkuu la kutoa muda wa mwezi mmoja kwa watumiaji wa malori na mabasi kuendelea kutumia sheria ya zamani, wakati ufumbuzi wa tatizo ukiwa bado unatafutwa.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Dk. Magufuli alitoa agizo la kuwataka wamiliki wa magari makubwa ya mizigo, kutozwa asilimia tano kwa kila gari litakalozidisha uzito, jambo ambalo lilipingwa vikali na wamiliki wa vyombo hivyo vya usafiri, hali iliyotishia uwepo wa mgomo wa watoa huduma ya usafirishaji kwa nchi nzima.

Kuibuka kwa mgomo huo kulisababisha hali ya upakuaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam kushuka kwa kasi, kutoka kontena 800 kwa siku hadi kontena 300 na hivyo kusababisha hasara inayokadiriwa kufikia kati ya Sh bilioni 20 na 30.

Kuendelea kwa mgomo huo, ambao ulitajwa kuwa ni tishio la uchumi, kulimfanya Pinda katikati ya wiki hii kulivalia njuga sakata hilo na kuruhusu malori na mabasi kuendelea na safari zao kama kawaida, wakati juhudi za kutafuta suluhu zikifanyika.

Katika agizo lake, Waziri Mkuu alisisitiza kwamba ni lazima pande zote mbili zikae chini na kufanya utafiti kuhusu mambo yanayolalamikiwa na kutoa jibu la kudumu na kusema kuwa kwa upande wa Serikali, itatoa timu ya wataalamu watakaofanya kazi na wawakilishi wa wasafirishaji ili kupata suluhu ya pamoja.

“Kwa hili suala, kuwashirikisha wadau ni jambo la msingi na busara kwa sababu uchumi wa nchi unategemea sekta hii, kwa kuwa asilimia 90 ya bidhaa zote, vikiwamo vyakula, vinasafirishwa kwa malori, huku asilimia 64 ya mizigo hiyo ikienda nchi jirani

“Hivyo hawa ni wadau wakubwa wa usafirishaji, inatupasa tuzungumze nao ili jambo hili limalizike…kumekuwapo mrundikano mkubwa wa shehena huko bandarini kutokana na meli kutoshusha mizigo, ndiyo maana tumeona tulimalize suala hili kwa mapana,” alisema Pinda.

Kauli hiyo ya Pinda imeonekana kumkwaza Dk. Magufuli, ambaye sasa ameamua kutekeleza majukumu yake kwa kufuata kile kinachoagizwa na Waziri Mkuu na si kwa mujibu wa sheria kama anavyosisitiza.

“Nalazimika kutii kile alichokieleza Waziri Mkuu, hata kama sikuridhishwa nacho,” alisema Dk. Magufuli.

Mwaka 2006, Wizara ya Ujenzi ilitoa barua kuruhusu malori kuzidisha mzigo juu ya kiwango cha mwisho cha uzito uliowekwa kisheria wa tani 56, lakini isiwe zaidi ya asilimia tano.

Hata hivyo, Wizara ya Ujenzi ikatoa barua nyingine mwaka huu, kwamba kuanzia Oktoba mosi, malori hayo yatii sheria inayotaka yasizidishe mzigo zaidi ya kiwango kilichowekwa kisheria cha tani 56.

Wakati hayo yakijiri, RAI Jumapili imedokezwa kwamba hali bado ni mbaya katika mizani za Kihonda, Mikese zilizopo mkoani Morogoro na ule wa Kibaha, mkoani Pwani, ambapo hadi jana kuliendelea kuwepo na foleni kubwa ya mlori ya mizigo.A

No comments:

Post a Comment